Wakati Rais wa Urusi Vladimir Putin akisifia “umoja na uzalendo” wa taifa hilo na kujaribu kuunda jeshi lililojumuishwa nyuma yake baada ya uasi ulioshindwa na mamluki wa Wagner, Warusi mnamo Jumanne waliendelea kukabili maswali juu ya mgawanyiko katika vikosi vya usalama na jinsi rais aliruhusu nchi kufikia hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ikulu ya Kremlin siku ya Jumanne ilifanya kazi kubwa kujaribu kuleta umoja na kurejesha nguvu ya Putin huku pia ikihamia kumtia doa Yevgeniy Prigozhin, mshirika wa zamani wa Putin ambaye aliongoza uasi,lakini maelezo rasmi ya kwanini Prigozhin aliruhusiwa kutoroka bila adhabu yalionekana kuwa yasiojitosheleza , ikionyesha mashaka mapya juu ya nguvu na uwezo wa Putin katika matatizo kama vita.
Rais wa Belarus Alexander Lukashenko alithibitisha Jumanne kwamba Prigozhin amewasili Belarus, sharti muhimu katika makubaliano yake na Kremlin kufuta mashtaka ya uasi dhidi yake na kuruhusu Wagner kuhamisha shughuli zake. Lukashenko alisema kuwa kundi hilo la mamluki litapewa kambi ya kijeshi iliyotelekezwa kwa matumizi yake.
Wizara ya Ulinzi ya Russia Jumanne pia ilitangaza kuwa hatua zinachukuliwa kwa Wagner kukabidhi silaha nzito ambazo serikali imewapa mamluki hao kuendesha vita nchini Ukraine.
Mapema Jumanne, Putin alikutana na kundi la maafisa wa kijeshi na usalama, ambao aliwasifu kwa kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe, baada ya mkutano wa usiku wa Jumatatu na viongozi wa mashirika yote makubwa ya usalama.
“Umelinda mfumo wa kikatiba, maisha, usalama na uhuru wa raia wetu, umelinda nchi yetu dhidi ya mishtuko na kusimamisha vita vya wenyewe kwa wenyewe,” Putin aliwaambia maafisa wa Wizara ya Ulinzi, Walinzi wa Kitaifa, Huduma ya Usalama ya Shirikisho (FSB).