Baada ya ripoti za Wanafunzi wa Kunduchi Girls Secondary kugoma wakiulalamikia Uongozi mpya wa Shule hiyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)-Makao Makuu imesema inafanyia uchunguzi malalamiko dhidi ya Viongozi wa Taasisi ya MDI inayomiliki baadhi ya Shule ikiwemo Shule hiyo ambapo pamoja na mambo mengine imeshindwa kuwalipa mishahara na posho nyingine Walimu na Wafanyakazi wengine.
Malalamiko mengine ni Mkurugenzi kukataa kulipa madeni ya Walimu na Wafanyakazi wengine ambayo hadi Mwezi huu yamefikia zaidi ya Milioni 400, pia Mkurugenzi wa MDI na Mkurugenzi mpya wa Elimu wa Shule hiyo wamekuwa wakiingia mikataba mibovu na kuikodisha Shule kwa Wamiliki mbalimbali bila kufuata utaratibu.
“Uongozi wa MDI unakwepa kodi na kuisababishia hasara Serikali na pia umetangaza kuwaondoa Walimu na Wafanyakazi wote bila kuwalipa malipo yao kwa madai kuwa hiyo ni amri kutoka Uongozi wa Mkoa, na tangu mwaka 2017 inalalamikiwa kuwa Bodi ya Wadhamini inaongoza Shule hiyo bila kusajiliwa RITA”– TAKUKURU
TAKUKURU imesema imeshafanya mahojiano na baadhi ya Walalamikaji na wanaendelea kuwahoji walalamikiwa, leo wamemuhoji Mkurugenzi wa MDI, Ally Magoga lengo likiwa ni kufahamu ukweli wa malalamiko haya ili hatua zichukuliwe.