Kiongozi wa zamani wa kundi la siasa kali za mrengo wa kulia la Proud Boys amehukumiwa kifungo cha miaka 17 jela kwa jukumu lake la kuvamia ikulu ya Marekani, ikiwa ni sehemu ya jaribio lililoshindwa la kupindua ushindi wa Rais Joe Biden katika uchaguzi wa 2020.
Hukumu hiyo ya Joseph Biggs, 33, ni kifungo cha pili kwa muda mrefu zaidi jela kutolewa kwa yeyote aliyehusika katika ghasia za Bunge la Merika mnamo Januari 6, 2021.
Biggs, pamoja na wanachama wengine watatu wa Proud Boys, walipatikana na hatia ya njama ya uchochezi na makosa mengine mwezi Mei.
Watu hao wanatuhumiwa kuzuia ubadilishanaji wa amani wa madaraka kutoka kwa Donald Trump hadi kwa Joe Biden, baada ya uchaguzi wa rais wa 2020.
Zaidi ya watu 1,106 wamefunguliwa mashtaka kuhusiana na ghasia za Capitol, ambapo wafuasi wa rais wa wakati huo Donald Trump walivamia kiti cha bunge la Marekani katika jaribio la kuzuia kukabidhiwa madaraka kwa amani.
Takriban 597 wametiwa hatiani na kuhukumiwa.