Watoto wawili wa familia moja ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi katika halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe wanadaiwa kubakwa na kuambukizwa virusi vya ukimwi (VVU) na baba yao wa kufikia.
Victor Nyato ni mwenyekiti wa mtaa wanapoishi watoto hao na mama yao ambao mmoja anasoma darasa la pili mwenye umri wa miaka 7 na mwingine anasoma darasa la tatu akiwa na umri wa miaka 10,amesema chanzo cha watoto hao kufanyiwa ukatili ni mama kutumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi za kusaidia fundi ujenzi na kunywa pombe.
“Mama ameniambia watoto wote amepata akiwa Dar es Salam na baba zao ni tofauti lakini baada ya kuona maisha ni magumu ndio akarudi Makambako akawa na mshkaji wake kilabuni akawa anamkimbia kilabuni na kwenda nyumbani kutekeleza ukatili huo”amesema Victor Nyato
Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Kipolisi Makambako Omary Diwani amethibitishia kutokea kwa tukio hilo na kupata taarifa Septemba 18,2024 baada ya bibi wa watoto kubaini wajukuu wake wamebakwa na mtuhumiwa akidaiwa kukimbia.
“Ni kweli kuna taarifa ya kufanyiwa vitendo hivyo na baba yao wa kufikia utaratibu wa kipolisi ulifanyika lakini bahati mbaya hili swala wao walitambua toka Septemba 11,2024 sasa lilichelewa kufika kwenye mamlaka na wakati tunafanya juhudi za kumpata mtuhumiwa alitoroka”amesema Omary Diwani
Ili watoto hao waweze kuishi kwa amani na uangalizi mkubwa,idara ya ustawi wa jamii Makambako imewahamishia watoto kwenye kituo cha kulelea watoto yatima lengo ikiwa ni kuhakikisha wanapata huduma bora hususani chakula na dawa.