Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imemuachia huru Jonas Charles maarufu Mkondo Abisai Mkazi wa Wilaya ya Sikonge aliyekuwa akikabiliwa na makosa ya kuua bila kukusudia.
Akisoma uamuzi huo wa Mahakama Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora Dkt. Mwajuma Kadilu Juma amesema Mahakama imepitia hoja za pande zote mbili katika shauri hilo na kubaini kuwa Mshtakiwa alitenda kosa hilo bila kukusudia.
Amesema kwakuwa ameshakaa muda wa zaidi ya miaka sita gerezani ambao unatosha kuwa adhabu, hivyo ameachiwa huru huku akitakiwa kwenda kuishi kistaarabu na jamii pasipo kutenda makosa ya aina hiyo.
Jonas alishitakiwa kumuua bila kukusudia kwa kumchoma kisu mara tatu Willson Kaswiza mwaka 2010.
Hata hivyo upande wa mashtaka chini ya wakili Tunosye Luketa uliiambia Mahakama kuwa, Mshtakiwa alitenda kosa hilo Juni 22 mwaka 2010 baada ya kumchoma kisu zaidi ya mara tatu marehemu Willson katika vurugu zilizotokea wakati wakiwa kwenye moja ya starehe Kijiji cha Kawale, Wilayani Sikonge.