Wabunge wamepitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 ya jumla ya shilingi Trilioni 34.88.
Bajeti hiyo imepitishwa kwa kura 304 za ndio kati ya kura 371 zilizopigwa na wabunge waliokuwepo bungeni jijini Dodoma.
Shughuli ya upigaji kura, imefanyika kwa mbunge kuitwa jina lake na kupiga kura hadharani kwa sauti.
Akitangaza matokeo ya kura, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amesema, wabunge waliopiga kura walikuwa 371 na wabunge 13 hawakuwepo bungeni.
Kagaigai amesema, kura 63 zimepigwa za ‘hapana’ na 304 wamepiga kura ya ‘Ndio.
Baada ya Kagaigai kumaliza kutangaza matokeo, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alisimama na kusema, “ni kura nyingi, rekodi haijapata kutokea. Kura zinaonyesha kwamba yajayo..” kisha wabunge wa chama tawala (CCM) wakaitikia kwa shangwe ‘yanafurahisha.’
Spika Ndugai ameipongeza Wizara ya Fedha na mipango chini ya waziri wake, Dk. Philip Mpango jinsi walivyotoa ushirikiano kwa Kamati ya Bunge na Bunge zima wakati wote wa uwasilishaji wa bajeti kwa miaka mitano mfululizo.