Balozi wa Africa Kusini nchini Tanzania, Mhe. Noluthando Mayende-Malepe ametembelea Taasisi za Victorious Center of Excellence na The Victorious Academy na kuonana na Mkurugenzi wake Bi Sarah Laiser-Sumaye.
Balozi, aliwapongeza wakurugenzi wa taasisi hizo kwa jitihada mbalimbali walizoziweka katika kuboresha huduma kwa watoto hawa wenye mahitaji maalum ambazo ni pamoja na kuajiri wataalam waliobobea katika fani hii kutoka mataifa mbalimbali yaliyopiga hatua katika kukabiliana na changamoto za usonji na utindio wa ubongo.
“Nawasihi wazazi kuacha tabia ya kuwaficha manyumbani watoto wenye hali ya usonji na utindio wa ubongo, pia waweke jitihada katika malezi sahihi ya watoto hawa kwa kutambua zaidi mahitaji na haki zao za msingi ikiwemo kupatiwa elimu stahiki, kufanyishwa mazoezi ya kiafya na kiakili sambamba na kuepushwa na unyanyapaa wa aina yoyote,”.
Kwa upande wake Sarah Laiser-Sumaye ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi hizo alimueleza Balozi changamoto zitokanazo na hali ya usonji kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na na ukosefu wa ufahamu katika jamii na imani potofu za kiasili zinazoambatana na hali hii. Kwa kuzingatia hili, taasisi za Victorious zinatoa ufahamu kwenye jamii kuhusu usonji pamoja na jinsi ya kukabiliana nayo.
Kwa mujibu Laiser takwimu za hapa nchini zinaonyesha ongezeko kubwa la tatizo la usonji katika miongo miwili iliyopita.
“Zaidi, tafiti hiyo ilibaini kati ya watoto 36 mmoja wao hubainika na tatizo la usonji, na pia kati ya watoto 4 wenye hali ya usonji mmoja wao ni wakike, hii inaonesha watoto wa kiume hupatwa na tatizo hili mara nne zaidi ya watoto wa kike huu ni wito wa kuchukua hatua, wito wa kujibu kwa huruma, uelewa, na kwa hatua madhubuti.’’ Alibainisha.
Kupitia Taasisi za Victorious, watoto wenye mahitaji maalum wanapata huduma mbalimbali za tiba za urekebishaji (rehabilitation therapies), elimu maalum pamoja na vocational training kwa lengo la kuwafanya waweze kujitegemea na kuwajumuisha katika jamii kupitia juhudi makini za kujenga uelewa kwenye kijamii na wazazi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu hatua mbalimbali za kukabiliana na hali ya usonji pamoja na maendeleo mapya zaidi ya tafiti yanayotokea ulimwenguni kote.