Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema hakuna Mtanzania aliyeambukizwa virusi vya Corona, anawasiliana na wanafunzi hao pamoja na Serikali ya China ili kufahamu na kutatua changamoto zinazowakabili.
Amesema kuishi kwa kufuata maelekezo ndilo jambo linalomfanya hata yeye kubaki hai, hawaruhusiwi hata kutoka nje na kwamba kitendo cha kukusanyika walichokifanya vijana waliosambaza video siku za hivi karibuni ni hatari sana kwa afya zao.
Kuhusu ombi la vijana hao kurejeshwa Tanzania, Balozi Kairuki amesema hakuna usafiri wowote unaoruhusiwa kutoka ama kuingia kwenye Mji wa Wuhan na kwamba Japan ilijaribu kuwaokoa vijana wake lakini wakaambukizwa virusi hivyo nchini kwao.
Amesema Virusi hivyo ni hatari na Serikali ya Tanzania haitafanya kitendo chochote kitakachokuja kuwadhuru Watanzania walio wengi, kitendo walichokifanya vijana hao kimetokana na msongo wa mawazo unaotokana na kukaa ndani ya uzio wa makazi yao bila ruksa ya kutoka nje.
Balozi Kairuki ametoa wito kwa Watanzania kuwaombea Watanzania wanaoishi China ili Mungu awavushe salama na kadhia hiyo, pia amewaomba wazazi kuwapa faraja vijana wao waliopo China ili waondokane na msongo wa mawazo.