Katika kuongeza ubora wa huduma za kadi, BancABC leo imezindua kadi mpya za malipo maarufu kama ‘Gusa ulipe’ ili kuwawezesha wateja wake kufanya malipo kwa urahisi, haraka na usalama. Teknolojia hiyo ni ya kisasa zaidi katika kufanya malipo na ni salama na ya uhakika kwa watumiaji.
Teknolojia hii inaleta mageuzi makubwa kwenye huduma za malipo kwani kwa sasa wateja wataweza kufanya malipo kwa urahisi zaidi kwa kugusisha kadi kwenye mashine ya POS tofauti na ile ya awali ya kuchanja (swipe) au kuchomeka kadi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Meneja Mkuu wa kadi na teknolojia za kidijitali wa benki hiyo, Bwana Lameck Mushi alisema kadi hizo zitaleta urahisi wa malipo kwa kadi kwa wateja na kupelekea uharaka wakati wa kufanya miamala hivyo kuboresha huduma za malipo kwa njia ya kadi.
“Kadi hizi za VISA zinatumia mfumo unaokuwezesha kufanya malipo ya haraka mahala popote na inaondoa ulazima wa kutembea na pesa taslimu ili kulipia huduma mbalimbali. Teknolojia hii inaongeza ufanisi wa malipo kwa wateja wetu kwa sababu mchakato wake ni rahisi na salama zaidi,” alisema bwana Mushi.
Mushi aliendelea kueleza kuwa, miamala itakayofanywa kwa kutumia teknolojia mpya ya gusa ulipe, ina usalama asilimia 100 dhidi ya uhalifu wa mitandaoni kwani bado inatumia ulinzi wa namba ya siri ya mteja (PIN) hususani kwa miamala ya malipo yenye thamani kubwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za uwakala wa benki na mahusiano ya kimkakati wa benki hiyo, Ndugu, Mwita Rhobi alisema “Mbali na kumuwezesha mteja kufanya malipo mtandaoni au kupitia mashine za POS BURE, kadi hizi zinaweza kutumika kwenye ATM zaidi 2,000 zinazopokea kadi ya VISA Tanzania. Pia, inaweza kutumika kwenye ATM zaidi ya milioni 2.7 zinazopokea kadi za VISA duniani na kupitia vituo zaidi ya 24,000 Tanzania vinavyopokea malipo ya kadi za VISA”
Mwita aliongezea kuwa, Kadi hizi zenye teknolojia ya gusa ulipe zinapatikana katika sarafu sita ikiwamo Shilingi ya Tanzania, Dola za Kimarekani, Randi ya Afrika Kusini, Euro, Pauni ya Uingereza pamoja na Yuan ya China.