Benki ya NCBA Tanzania, taasisi ya kifedha inayoongoza nchini, imetangaza mipango yake ya kutanua shughuli zake ili kugusa sekta zote muhimu za kiuchumi zikiwemo FMCG, usafirishaji, nishati na viwanda.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa kwa ajili ya wateja wao, Mkurugenzi Mkuu wa NCBA Group alisema, “Tumegundua kuwa ukuaji wa Tanzania unatokana na ukuaji wa sekta hizi muhimu za kiuchumi na tunataka kuwa sehemu ya ukuaji huo.”
Pia aliongezea kwa kusema kuwa Benki ya NCBA imejipanga vyema kuwezesha ukuaji wa biashara nje ya mipaka na uwepo wa benki hiyo katika nchi jirani ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Ivory Coast.
Licha ya changamoto zinazoletwa na janga la Uviko-19, Benki ya NCBA Tanzania imeendelea kuimarika, hasa kutokana na benki ya NCBA kufikia masoko mbalimbali na ongezeko la bidhaa zake za kidijitali, ikiwemo M-Pawa, ambayo imehudumia takribani wateja milioni 7. Benki hiyo imejitolea kutoa huduma za kifedha kwa watu wasio wateja wa benki, na juhudi zake zimetambuliwa kwa tuzo ya benki bora zaidi katika maswala ya kidijitali nchini.
Benki ya NCBA Tanzania imejipanga kuwahudumia wateja wake na kufanikisha makubwa pamoja. Hivi majuzi benki ilipokea nyongeza ya Bilioni 40 ya mtaji kutoka kwa wanahisa wa NCBA Group, ikiwa ni rasilimali muhimu katika mpango wake kukua na kutanua masoko zaidi.
Mh. Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Charles Mwamwaja ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo na kuunga mkono dira ya Benki ya NCBA Tanzania katika kuwahudumia watanzania. Wakati huo huo, benki ilimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wake mpya, Bw. Claver Serumaga kuongoza njia kufika makubwa Zaidi.
Mipango ya Benki ya NCBA Tanzania ya kujitanua katika sekta muhimu za kiuchumi na kuendelea kuongeza ubunifu wa kidijitali inaonyesha dhamira ya benki hiyo katika kukidhi mahitaji ya wateja wake na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini Tanzania na kwingineko.