Baraza la mawaziri la vita la Israel lilifanya mkutano kujadili na kuamua jinsi watakavyojibu mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran. Israel haikutangaza ikiwa wamefikia uamuzi.
Hatua hizo za Iran zililaaniwa vikali na washirika wa Israel, hata hivyo, serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilitolewa wito na nchi hizo kuonyesha kujizuia.
Ingawa Iran imeashiria kwamba inazingatia suala hilo kufungwa, mkuu wa jeshi la Israel Lt Jenerali Herzi Halevi alisema kuwa shambulio hilo halitapita bila kujibiwa.
“Uzinduzi huu wa makombora mengi, makombora na ndege zisizo na rubani katika ardhi ya Israeli utakabiliwa na jibu,” alisema Halevi, wakati akizungumza kutoka kambi ya Jeshi la Wanahewa la Nevatim kusini mwa Israeli, ambayo pia ilipata uharibifu kidogo katika shambulio hilo.
Tangu shambulio hilo, huu ndio uthibitisho wa wazi zaidi uliotolewa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Israel Lt Jenerali Herzi Halevi kwamba Israeli ingejibu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala ya Kisiasa, Ali Bagheri Kan alisisitiza kwamba kasi ya kukabiliana na Iran “itakuwa chini ya sekunde chache.”
Katika siku mbili zilizopita, baraza la mawaziri la vita la Israel lilifanya mkutano kwa mara ya nne huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akijadili tena kile kinachopaswa kuwa hatua inayofuata na Waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant, na Benny Gantz, waziri wa zamani wa ulinzi na mpinzani mkuu Netanyahu.