Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) leo tarehe 16 Aprili, 2024 limepokea mapendekezo ya uteuzi wa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo katika Kikao chake cha 52 cha Dharura kilichofanyika kwa njia ya mtandao.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato (Mb.) akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika mashariki, Balozi Stephen Mbundi.
Mapendekezo hayo yamewasilishwa kufuatia mabadiliko ya nafasi hiyo yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Samoei Ruto ambapo amemteua Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Dkt. Peter Mutuku Mathuki kuwa Balozi wa Jamhuri ya Kenya nchini Urusi.
Hivyo, Mhe. Ruto amempendekeza Bi. Veronica Mueni Nduva kuchukua nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya mara baada ya kuthibitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katibu Mkuu wa Jumuiya huteuliwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa Mkuu wa Nchi husika kulingana na utaratibu wa mzunguko ambao unatoa kipindi cha miaka mitano ya kuhudumu katika nafasi hiyo.
Katibu Mkuu wa sasa Dkt. Peter Mathuki aliteuliwa na Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 27 Februari, 2021. Hivyo, kulingana na muda wa kuhudumu Jamhuri ya Kenya imebakiwa na miaka miwili kukamilisha kipindi chake cha miaka matano (5).