Baraza la Seneti la Ufaransa Jumatano liliidhinisha muswada wa sheria wa kuweka katika katiba ya nchi haki ya mwanamke kutoa mimba, na kuondoa kikwazo kikubwa kwa sheria iliyoahidiwa na Rais Emmanuel Macron ili kukabiliana na athari za hatua ya kubatilisha haki ya utoaji mimba Marekani.
Kura hiyo ya Baraza la Seneti inajiri baada ya Bunge la taifa kuidhinisha kwa kishindo muswada huo mwezi Januari.
Muswada huo sasa utawasilishwa mbele ya kikao cha pamoja cha bunge ili uidhinishwe na theluthi tano za wabunge wiki ijayo.
Macron alisema baada ya kura hiyo kwamba serikali yake ina dhamira ya “kufanya haki ya utoaji mimba kwa wanawake iwekwe bila pingamizi katika katiba ya nchi.” Alisema kwenye mtandao wa X kwamba ataitisha kikao cha pamoja cha bunge kwa ajili ya kura ya mwisho Jumatatu.
Baraza la Seneti lilipitisha muswada huo kwa kura 267 dhidi ya 50.