Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotaka kusitishwa kwa haraka na kuongezwa muda wa kusitisha mapambano huko Gaza.
Azimio nambari 2712 linatoa wito wa kusitishwa kwa haraka na kuongezwa muda wa kusitisha mapambano kwenye ushoroba wa Ukanda wa Gaza kwa siku kadhaa za kutosha ili kuwezesha ufikiaji kamili, haraka, salama na usiozuiliwa wa kibinadamu, kuwezesha utoaji endelevu, wa kutosha na usiozuiliwa wa bidhaa na huduma muhimu kote Gaza, zikiwemo maji, umeme, mafuta, chakula na vifaa vya matibabu, pamoja na ukarabati wa dharura wa miundombinu muhimu; na kuwezesha juhudi za dharura za uokoaji na ufufukaji, zikiwa ni pamoja na kutafuta watoto waliopotea katika majengo yaliyoharibiwa, na kuwahamisha watoto wagonjwa au waliojeruhiwa na walezi wao.
Azimio hilo limeungwa mkono na wajumbe 12 kati ya 15 wa baraza hilo, ambapo Uingereza, Russia na Marekani hazikupiga kura.
Azimio hilo linazitaka pande zote kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria za kibinadamu za kimataifa, hasa kuhusu ulinzi wa raia, hususan watoto.