Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania linatarajia kuendesha zoezi la Mtihani kwa watahiniwa 4165, ambao wamekidhi vigezo vya kufanya Mtihani huu, wakiwemo waombaji 3917 ambao wanafanya mtihani kwa mara ya kwanza na 248 wanaorudia. Kati yao, Wanaume ni 1647 na wanawake ni 2518.
Hayo yamesemwa na Kaimu Msajili Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Happy Masenga, leo Disemba 28, 2023, wakati akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa ofisi za Baraza hilo Jijini Dodoma.
Aidha, Mtihani huu utafanyika katika vituo vilivyotambuliwa na kukubaliwa na Baraza katika Mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, na Tabora siku ya Ijumaa 29/12/2023, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana.
Lengo la Mtihani huu ni kupima umahiri wa watahiniwa ili kupata wataalamu wa Afya wenye sifa za kusajiliwa na kupewa leseni ya kutoa huduma kama Muuguzi au Mkunga kwa mujibu wa kifungu cha 15 (1) (a-b) cha Sheria ya Uuguzi na Ukunga.
Mtihani wa usajili na leseni umekuwa ukifanyika tangu kuanzishwa kwa Baraza mwaka 1953 kwa mujibu wa kifungu 6 (a) cha Sheria, ambapo hapo awali mtihani huu uliendeshwa kwa ushirikiano kati ya Baraza na Wizara ya Afya.
Baraza la Uuguzi na Ukunga Nchini lina jumla ya wauguzi na wakunga wenye leseni wapatao 49,994, ambao wanatoa huduma kwenye Hospitali za Rufaa, Mikoa, Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati.