Mabingwa wa zamani wa Hispania na Ulaya, FC Barcelona wako kwenye mgogoro mzito ambao unatishia kupotea kwa amani ndani ya klabu hiyo.
Hali ndani ya Nou Camp katika kipindi cha saa 48 zilizopita imekuwa mbaya kufuatia matokeo mabaya ambayo klabu hiyo imeyapata hivi karibuni hasa kwenye mchezo wao wa kwanza kwa mwaka 2015 ambao walijikuta wakifungwa na vijana wa David Moyes, Real Sociedad.
Makamu wa Rais wa Barcelona, Josep María Bartomeu ambaye amekuwa akikaimu nafasi ya rais tangu kuondoka kwa Sandro Rossel ambaye aliwajibika kutokana na kashfa ya usajili wa Neymar amejikuta akiwa hana la kufanya kutatua mgogoro uliojitokeza hivi karibuni huku shinikizo juu yake kuwajibika likizidi kuongezeka siku hadi siku.
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita Barcelona imemfukuza kazi Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Barca na timu ya taifa, Andoni Zubizaretta huku dakika chache baada ya kufukuzwa kwake msaidizi wake kwenye nafasi hiyo, Carles Puyol naye akiamua kuachia ngazi.
Zubizaretta amelaumiwa kwa kusajili wachezaji ambao wameshindwa kuonyesha kiwango cha juu hadi sasa akiwemo Luis Suarez ambaye bado hajaweza kuonyesha makali kama aliyokuwa akiwa na Liverpool.
Matokeo mabaya yamefanya nafasi ya kocha Luis Enrique kuwa hatarini huku akipewa mechi mbili za kuhakikisha anashinda au kufukuzwa kazi.
Taarifa za ndani ya Barcelona zinasema kuwa uongozi wa klabu hiyo uko kwenye hali ya majuto kutokana na kutambua kuwa ulifanya makosa kumuajiri Luis Enrique ambaye ameonekana kukosa uzoefu wa kuwaongoza wachezaji nyota huku akilaumiwa kwa kitendo cha kuwaanzisha kwenye benchi nyota wawili wa timu hiyo Lionel Messi na Neymar.
Vyanzo kadhaa vimedai kuwa mchezaji bora wa dunia mara nne Messi amekuwa hana raha ndani ya Barcelona hivi karibuni na hali hii huenda ikamfanya awekwe sokoni japo Barcelona mara kadhaa imekanusha taarifa za kutaka kumuuza.
Lionel Messi hakuonekana kwenye mazoezi ya Barcelona ya jumatatu kitendo ambacho kimesaabishwa na maamuzi ya kuachwa kwenye benchi kwenye mchezo dhidi ya Sociedad japo aliingizwa hapo baadae.
Kundi kubwa la wachezaji wa Barca wamemlalamikia kocha Luis Enrique huku wakisema kuwa hawafahamu mustakabali wao ndani ya klabu hiyo kwa kuwa kocha hawajawaeleza juu ya nafasi walionayo kwake.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook