Klabu ya Barcelona imeliomba shirikisho la soka barani ulaya UEFA kutojumuisha jina la kiungo wake wa zamani Luis Figo katika orodha ya wachezaji wake wa zamani ambao walipangwa kushiriki kwenye mchezo wa kirafiki kati ya timu inayoundwa na wachezaji wa zamani wa Juventus na Barcelona dhidi ya timu ya dunia uliopangwa kufanyika wiki hii .
Hatua hii inakuja baada ya mashabiki wa Barca kuandamana wakionyesha hasira zao kwa kitendo cha mchezaji huyo kuihama klabu yao na kujiunga na mahasimu wao kwenye soka la Hispania Real Madrid miaka 15 iliyopita .
Figo kabla ya hapo alicheza kwenye uwanja wa Nou Camp kwa miaka mitano kabla ya kuhamia Santiago Bernabeu mwaka 2000 na kitendo hiki bado hakijasahaulika akilini mwa mashabiki wa Barcelona ambao wameonyesha hisia zao.
Mchezo ambao Barcelona imeomba jina la Figo litolewe utahusisha timu mseto yenye wachezaji wa zamani wa Juventus na Barcelona dhidi ya timu yenye mchanganyiko wa wachezaji wa zamani toka mataifa na klabu tofauti ikiwa ni moja kati ya matukio ya awali kuelekea kwenye mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa barani ulaya itakayopigwa Jumamosi hii huko Berlin .
Figo alichezea klabu hizi mbili kwa kipindi cha miaka kumi kati ya mwaka 1995 na 2005 ambapo alihamia Inter Milan ya Italia .
Hivi karibuni Figo aliingia kwneye kinyang’anyiro cha kuwania urais wa shirikisho la soka duniani Fifa kabla ya kujitoa kuelekea mwishoni mwa uchaguzi huo .