Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS) kumuondoa Mkandarasi wa kampuni ya Kay Bouvet Engineering Ltd ya nchini India na kumtafuta Mkandarasi mwingine mwenye uwezo na sifa za kujenga miundombinu ya barabara katika Kiwanda cha sukari cha Mkulazi Mkoani Morogoro.
Waziri Bashungwa ameeleza hayo wakati akikagua ujenzi wa kiwanda na miundombinu ya barabara katika Kiwanda cha Sukari na Shamba la Mbigiri na kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo.
“Jukumu la TANROADS ni kusimamia ujenzi wa kiwanda hiki katika miundombinu ya barabara lakini Mkandarasi huyu ni mbabaishaji, na tumeamua kumuondoa kwa kuwa hana mitambo ya kutosha ya kutekeleza kazi ya ujenzi wa barabara pia hana sifa na uzoefu wa barabara kwa kiwango cha lami”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta kutangaza zabuni ya mradi huo mara moja na kumpata Mkandarasi mwenye sifa na uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi mkubwa mradi huo.
Bashungwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya kiwanda hicho kilichofikia asilimia 70 kutasaidia kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kulisaidia Taifa kuzalisha sukari ya kujitosheleza kupitia Viwanda vya ndani.
Kadhalika, Waziri Bashungwa, amemshukuru Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya Ujenzi wa viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Sukari cha Mkulazi ambacho kitakuwa na uwezo wa kusaga tani 2,500 za miwa na kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka.