Katika ufuatiliaji wangu wa mahojiano yanayofanywa na CNN kwa Waafrika mbalimbali katika African Voices, hii ya Bayi nayo imenifurahisha kwa jinsi alivyotumia muda mfupi aliopewa kujieleza yeye mwenyewe lakini pia kuipa shavu nchi yake kwa kuupa nafasi mlima Kilimanjaro.
Mara nyingi huwa inatokea na inawezekana ni bahati mbaya, Waafrika wengine wanapohojiwa wanaweza kujisahau na kuzungumzia mambo yao zaidi bila kuitumia hii nafasi ya chombo kikubwa cha habari ulimwenguni kama hiki kuhusisha mazungumzo ya kutangaza zaidi nchi zao.
Filbert Bayi alitisha pale alipohusisha zaidi ya dakika moja kwenye kuuzungumzia Mlima kilimanjaro pamoja na picha zake kuonyeshwa huku akichomekea na stori ya shule zake zinavyotumia Mlima huo kufundishia Wanafunzi.
Pamoja na ishu nyingine Filbert Bayi ambae aliwahi kuwa Mwanariadha wa Tanzania alieipa nchi headlinez za ujazo duniani amethibitisha ni kweli ana miliki shule tatu sasa hivi baada ya safari ndefu aliyoianza kwa kuanzisha shule kwenye jengo la kuhifadhia magari nyumbani kwake (garage).
Anasema yeye na mke wake walianza na wanafunzi 35, mwaka 1997 na 1998 ambapo wakati huo mke wake pamoja na biashara nyingine alikua anamiliki saluni kwa ajili ya Wanawake.
Bayi ambae pia amemshukuru na kumzungumzia Rais Kikwete pale alipomuita na kufanya nae mazungumzo, amesema anachopenda kukiona kinatokea kwenye maisha yake siku moja ni kuwa na University inayofundisha Madaktari au Mainjinia.
Bayi hakuwahi kumuona baba yake kwa sababu alifariki kabla hajazaliwa hivyo alilelewa na mama yake tu.
Shule yake inawasaidia Wanafunzi wapatao 15 ambao wazazi wao walifariki dunia.
Kingine alichosema ni kwamba Watanzania wengi huwa wanafanya mazoezi Jumapili tu tena sio kwa ajili ya mashindano bali mazoezi tu kitu ambacho ni tofauti na Kenya wanakofanya mazoezi ya riadha kila siku kwa ajili ya kushiriki mashindano, mazoezi ambayo kwa kiasi kikubwa yamewapa ushindi.