Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kupanda kwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa Nchini zitakazotumika kuanzia leo Jumatano April 03, 2024 saa 6:01 usiku ambapo kwa mwezi April 2024, bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es Salaam petrol ni Tsh. 3257 kwa lita, dizeli Tsh. 3210 na mafuta ya taa 2840.
EWURA imesema kwa mwezi April 2024, mabadiliko ya bei yamechangiwa na kuongezeka kwa bei za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la dunia kwa wastani wa 3.94% kwa mafuta ya petroli na wastani wa 2.34% kwa mafuta ya dizeli, kupungua kwa gharama za kuagiza mafuta (premiums) kwa wastani wa 4.28% kwa mafuta ya petroli na kuongezeka kwa wastani wa 0.76% kwa mafuta ya dizeli kwa bandari ya Dar es salaam, kuongezeka kwa wastani wa 13.73% kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa Bandari ya Tanga na kuongezeka kwa wastani wa 12.71% kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa Bandari ya Mtwara.
“Aidha, mabadiliko hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa kiwango cha kubadilishia fedha za kigeni kwa asilimia 3.19 kutokana na ongezeko la matumizi ya EURO kulipia mafuta yaliyoagizwa”
Itakumbukwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini kwa mwezi uliopita zilizoanza kutumika kuanzia Jumatano March 06, 2024 saa 6:01, bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es salaam petrol ilikuwa ni Tsh. 3163 kwa lita, dizeli Tsh. 3126 na mafuta ya taa 2840.