Kuanzia sasa, abiria nchini China wataweza kulipia tiketi ya treni ya chini ya ardhi (Metro) kwenye mojawapo ya njia za usafiri huo mjini Beijing kwa kuskani kiganja cha mkono tu.
Kampuni ya Metro ya mji wa Beijing imetangaza kuwa imeanza kutoa huduma maalumu kwa abiria wake ya kuskani kwa muda mchache mno kiganja cha mkono ili kulipia nauli ya treni ya chini ya ardhi.
Gazeti la Beijing limeandika kuhusiana na suala hilo kwamba: huduma ya scanning kwa kiganja cha mtu cha mkono ni mwafaka zaidi kwa watu walio wazee kiumri, wale wenye matatizo ya kimwili, abiria waliosahau kadi zao za Metro au wale ambao hawawezi kutumia simu za mkononi, ambapo wote hao wanaweza kulipia nauli ya usafiri huo kwa njia hiyo.
Huduma za malipo kwa njia ya kuskani kiganja cha mkono zimepangwa kutolewa katika ofisi, maskuli, kumbi za michezo na mikahawa kwenye maeneo mbalimbali ya China.
Kwa msaada wa teknolojia za kisasa, China inaendelea kila uchao kuboresha utoaji wa huduma katika vituo na maeneo ya umma.
Katika mwendelezo wa utoaji huduma hizo, mnamo mwaka uliopita baadhi ya njia za metro katika mji wa Shenzhen zilizindua mashine za kuskani sura ya mtu kwa ajili ya kulipia nauli ya metro; na mwaka huu, treni ya chini ya ardhi ya Beijing imezindua huduma hiyo kwa kutumia mfumo wa kuskani kiganja cha mkono.
vyanzo mbalimbali vya habari.