Moja ya habari gumzo za wiki hii ni hii ya Wabunge wa Nchini Benin kupiga kura ya kuhalalisha utoaji mimba ambapo sasa Wanawake wa Nchi hiyo wanaweza kutoa mimba ndani ya miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito kama wameona ujauzito huo unaweza kuwasababishia matatizo mbalimbali kwenye elimu, kazi, maadili au kama Mtoto huyo anaetarajiwa anaweza kuathiri maisha ya Mama.
Hata hivyo utoaji mimba kwenye Taifa hili la Afrika Magharibi ambako Wanawake karibu 200 hufariki kila mwaka wakati wakitoa mimba, ulikua ukiruhusiwa hapo kabla lakini kwa kesi maalum tu ambazo ni kama Mwanamke amebakwa, maisha ya mama yalikuwa hatarini kwasababu ya ujauzito au afya ya Mtoto aliyetarajiwa kuzaliwa itaathirika.
Sheria mpya ambayo imepitishwa wiki hii na kuligawa Taifa hilo pande mbili huku wengine wakikubali na wengine kukataa bado itasubiri kupitishwa kikatiba Mahakamani kabla ya kuanza kutekelezwa, pamoja na hayo imeungwa mkono na Viongozi mbalimbali wa Nchi hiyo akiwemo Waziri wa afya aliyesema italeta unafuu kwa Wanawake wengi ambao wanapata ujauzito wasioutaka.