Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza kuwa wanajeshi wake watasonga mbele katika mji wa Rafah huko Gaza, na kukaidi maombi ya nje ya kutaka kutafakari upya.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikuwa miongoni mwa watu waliomwonya Bw Netanyahu, akimwambia kwamba gharama ya kibinadamu ya operesheni ya Israel huko Gaza “haivumiliki”.
Lakini Bw Netanyahu ameamuru jeshi lake kujiandaa kwa shambulio la ardhini.
Takriban Wapalestina milioni 1.4 wanajihifadhi katika mji wa Rafah, ambao tayari umeshambuliwa kwa mabomu.
Bw Netanyahu aliapa kuendelea na mashambulizi “ya nguvu”, akitangaza kwamba Hamas, kundi linalodhibiti Gaza, lazima liondolewe katika mji huo wa kusini.
“Tutapigana hadi ushindi kamili na hii inajumuisha hatua kali pia huko Rafah baada ya kuruhusu raia kuondoka kwenye maeneo ya vita,” alisema.