Benki kuu ya Libya imetangaza kusimamisha shughuli zake zote baada mfanyakazi wake wa ngazi ya juu kutekwa nyara katika mji mkuu Tripoli.
Benki hiyo ililaani kutekwa nyara kwa mkurugenzi wake wa teknolojia ya habari Musab Msallem katika taarifa yake siku ya Jumapili.
Imesema Bw Msallem alichukuliwa kutoka nyumbani kwake na “watu wasiojulikana” Jumapili asubuhi na kwamba wafanyakazi wengine pi wametishiwa kuteka nyara.
Benki kuu inasema shughuli hazitaendelea hadi Bw Msallem aachiliwe.
Benki kuu, ambayo ni huru lakini inayomilikiwa na taifa la Libya, ndiyo hifadhi pekee inayotambulika kimataifa kwa mapato ya mafuta ya Libya ambayo ni muhimu ya kiuchumi kwa nchi iliyosambaratishwa kwa miaka inayoongozwa na serikali mbili hasimu za Tripoli na Benghazi.
Hii inakuja wiki moja baada ya benki kuu kuzingirwa na watu wenye silaha, kulingana na shirika la habari la AFP.
Tangu kuondolewa madarakani na kuuawa kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi mwaka 2011, nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama.