Katika mwendelezo wa kusaidia jitihada za Serikali kukuza ujumuishi wa kiuchumi nchini, Benki ya CRDB leo imeingia mkataba wa makubaliano na Tume ya TEHAMA (ICTC), na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia programu yake ya ‘IMBEJU’ iliyojikita katika uwezeshaji wa wanawake na vijana kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema ushirikiano na taasisi hizo za Serikali utasaidia kufanikisha malengo ya programu kwa kiasi kikubwa kutokana na jinsi uzoefu wa taasisi hizo katika kuwawezesha vijana wabunifu katika sekta mbalimbali.
“Ili kuifanya programu hii kuwa yenye ufanisi na kufikia walengwa wengi, tumeona ni vyema kutafuta wadau ambao wana mawazo kama yetu yaani “like-minded partners”. ICTC na COSTECH wamekuwa wakifanya kazi nzuri ambayo inaakisi utayari wa Serikali yetu katika kukuza biashara na mawazo ubunifu, hivyo tunajivunia kwa hatua hii muhimu,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema mkataba wa makubaliano waliongia na Benki ya CRDB utakwenda kusaidia upatikanaji wa mitaji wezeshi kwa biashara changa katika sekta ya TEHAMA, pamoja na kutoa usaidizi wa kuboresha mawazo na biashara bunifu, jambo litakalosaidia kukuza ajira nchini.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Amos Nungu amesema makaubaliano waliyoaingia na Benki ya CRDB yanakwenda kuoanisha IMBEJU na programu za taasisi hiyo zinazochochea ubunifu wa kibiashara ikiwamo MAKISATU jambo litakalosaidia kuchochea kasi ya ukuaji wa biashara changa katika sekta mbalimbali.
Katika hafla hiyo, Benki ya CRDB pia iliutangazia umma kuanzishwa kwa taasisi isiyo ya faida ya “CRDB Bank Foundation” yenye jukumu la kuanzisha na kutekeleza programu bunifu, endelevu, na shirikishi zinazolenga kuleta ustawi wa kijamii, na kiuchumi kama ‘IMBEJU’.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alimtambulisha Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa kama Mkurugenzi Mtendaji mwanzilishi wa taasisi hiyo ya CRDB Bank Foundation.
Akizungumza kwa mara ya kwanza kama Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Mwambapa amewataka vijana wabunifu kuchangamkia fursa inayotolewa na benki hiyo kupitia programu ya IMBEJU inayotekelezwa kwa kushirikiana na ICTC, na COSTECH.
“Mkataba tulioingia leo unatupa uwezo wa kushirikiana na ICTC na COSTECH kufanya utambuzi wa biashara changa bunifu zinazohitaji usaidizi. Niwaombe vijana kutumia mifumo ya utambuzi ya taasisi hizi ili kunufaika na fursa hii,” amebainisha Tully.
Mwambapa alitumia fursa hiyo pia kuwaalika vijana kushiriki semina maalum ya uwezeshaji iliyoaandaliwa na Benki ya CRDB tarehe 11 Machi 2023 katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere, ambapo programu hiyo itaingizwa sokoni rasmi, na uwezeshaji kuanza kufanyika. Mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.