Benki ya Dunia imetoa taarifa ikisema inaunga mkono hatua ya Serikali ya Tanzania ya kuwaruhusu Wanafunzi wajawazito kurudi Shuleni na kusema itashirikiana na Tanzania kuifanya elimu kuwa bora kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kauli ya Benki ya Dunia inakuja kufuatia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kusema Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari watakaokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba na changamoto mbalimbali za kifamilia watapewa fursa ya kurejea Shuleni katika mfumo rasmi.
Benki ya Dunia imesema uaumuzi huu unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali kusaidia Wasichana kwa kuziboresha nafasi zao za kupata elimu bora.
Benki ya dunia imesema zaidi ya Wasichana 120,000 huacha Shule kila mwaka nchini Tanzania huku 6,500 kati yao ikiwa ni kwasababu ni Wajawazito au wana Watoto.