Benki kubwa ya biashara nchini Ethiopia inasema imefanikiwa kupata zaidi ya robo tatu ya pesa ilizopoteza baada ya hitilafu ya kiufundi kuwawezesha wateja kutoa au kuhamisha pesa zaidi ya walizokuwa nazo kwenye akaunti zao.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne mkuu wa Benki ya Biashara ya Ethiopia Abe Sano alisema zaidi ya $14m (£11m) zilitolewa kutoka kwa mashine za ATM au kuhamishiwa kwenye akaunti nyingine wakati wa tukio hilo la tarehe 16 Machi.
Zaidi ya $10m tayari zimepatikana, Bw Abe alisema. Ripoti za awali za vyombo vya habari vya ndani zilisema kiasi cha pesa zilizochukuliwa wakati wa hitilafu hiyo kinaweza kufikia hadi $40m.
Pesa nyingi zilichukuliwa na wanafunzi wa chuo kikuu.
Kulingana na mkuu wa benki hiyo, maelfu ya wateja walirudisha pesa hizo kwa hiari.
Aliongeza kuwa wale ambao hawajafanya hivyo wanaweza kukabiliwa na mashtaka ya jinai.