Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wakimbizi UNHCR limetoa wito wa kuwasaidia wakimbizi waliopo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC ambao wapo katika hali mbaya kutokana na kuendelea kwa machafuko yanayofanywa na makundi yenye silaha hali inayofanya watu kuyakimbia makazi yao.
Taarifa iliyotolewa jumanne na UNHCR kutoka Geneva Uswisi imesema ukosefu wa amani huko mashariki mwa DRC umesababisha watu kuwa na hali mbaya ya kimaisha na ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia, unaowakabiliwa zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni 6.2.
UNHCR na washirika wa misaada ya kibinadamu wameeleza kusikitishwa sana na ongezeko la unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana katika maeneo yenye msongamano wa watu kuyahama makazi yao.
Wameeleza wasiwasi mkubwa ni mwelekeo wa kuongezeka kwa ushiriki wa biashara ya ngono kutokana na uhaba wa chakula unaokabili kaya zilizohamishwa.
Wakati ukosefu wa usalama ukiendelea na mapigano makali yanaendelea kukumba eneo hilo, fursa kwa watu waliohamishwa kurejea makwao na maisha yao kwa usalama na utu bado ni finyu.
Rasilimali za ziada zinahitajika kwa haraka ili kuendelea kusaidia familia zilizohamishwa nchini DRC.
Kwa mwaka 2023, UNHCR hadi sasa imepokea asilimia 29 tu ya dola milioni 233 zinazohitajika kukidhi mahitaji ya watu waliokimbia makazi nchini humo.
CHANZO:UN