Joe Biden ametetea uamuzi wake wa kusalia kwenye kinyang’anyiro cha urais baada ya kuandamwa na wito wa kujiuzulu kufuatia utendaji wake duni katika mdahalo wa TV na Donald Trump.
Katika mahojiano na mtandao mshirika wetu wa NBC News wa Marekani, rais huyo wa Marekani alikuwa mbishi wakati fulani na kusema hatajiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho licha ya wito kutoka ndani ya chama chake kumtaka afanye hivyo.
“Mimi ni mzee – lakini nina umri wa miaka mitatu tu kuliko Trump, nambari moja, na nambari ya pili, akili yangu imekuwa nzuri sana,” Bw Biden alisema, alipokuwa akikabiliwa na maswali kuhusu umri wake.
“Nimefanikiwa zaidi kuliko rais yeyote amefanya kwa muda mrefu, mrefu katika miaka mitatu na nusu. Kwa hivyo niko tayari kuhukumiwa juu ya hilo,” alisema.
Mahojiano na Lester Holt wa NBC yalipangwa kabla ya jaribio la kumuua Donald Trump siku ya Jumamosi.
Biden alisema mamilioni ya wapiga kura wa Democratic wamemchagua kupitia kura za mchujo na alikuwa akiwasikiliza.