Kukamilika kwa Mfumo wa Makasha (kontena) yanayotumia umeme kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa ambazo zinaweza kuharibika kutokana na joto kumeelezwa kuwa kutawasaidia Wakulima na Wafanyabiashara mbalimbali wanaotaka kusafirisha bidhaa hizo kwenda nje ya Nchi kupitia Bandari ya Tanga, Kusafirisha bidhaa hizo bila kuharibika/kuoza.
Afisa Masoko na Huduma kwa Wateja wa Bandari ya Tanga Habiba Godigodi amesema hayo wakati wa Maonesho ya Wakulima Nanenane Kanda ya Mashariki Mjini Morogoro ambapo amesema Bandari hiyo imeamua kuja na ubunifu wa kontena hizo ambazo kwa sasa zipo 50, hivyo hata mzigo ukikaa siku nyingi bidhaa haziharibiki.
Habiba amesema kuwa kulikuwa na changamoto kwa Wakulima wanaosafirisha bidhaa kama matunda, nyama, maua na nyingine zinazoharibika kushindwa kusafirisha bidhaa hizo kutokana na kutokuwepo kwa njia sahihi ya kuhifadhi bidhaa hizo hivyo Bandari ya Tanga imetengeneza eneo maalum la kuhifadhia kontena zenye mfumo wa umeme ili waweza kuhifadhi wakati wanapotaka kusafirisha bidhaa hizo.
Moja ya kati ya changamoto ambazo Wakulima na Wafanyabiashara hukutana nazo wanaposafirisha bidhaa zao kama matunda, vyakula , maua n.k ni kuharibika/kuoza pale zinapokaa kwenye kontena, hivyo kontena hizo za umeme zitasaidia kuondokana na changamoto hiyo.