Katika kusheherekea siku yake ya kuzaliwa, mkurugenzi wa kampuni ya Mati Super Brands ltd David Mulokozi ametoa misaada mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanaolelewa katika kituo cha Hossana.
Akikabidhi misaada hiyo Meneja rasilimali watu Doreen Mushi amesema ni desturi ya Mulokozi kila anapokumbuka siku yake ya kuzaliwa kusheherekea na makundi maalum wakiwemo wazee na watoto yatima.
Misaada iliyokabidhiwa ni mahindi gunia moja, sabuni, nguo za shule,masweta, masufuria, mchele kilo 100, maharage kilo 100,mafuta ya kula,mafuta ya kujipaka, juisi,madaftari, beseni,ndoo,kalamu,sukari kilo 100 pamoja na kuwaunga mkono katika ujenzi wa kituo kwa kutoa matofali na nondo, kodi ya mwaka mmoja katika kituo kinachotumika kwa sasa ambavyo vyote vimegharimu shilingi milioni 12.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Hossana Neema Munis ameishukuru kampuni hiyo kwa misaada waliyokuwa wakiitoa kituoni hapo mara kwa mara.
Munis amesema kwa sasa mahitaji makubwa ni vifaa vya ujenzi wa kituo hivyo amewakaribisha watu wenye mapenzi mema kusaidia kwa chochote walichojaliwa ili kufanikisha.