Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa Shilingi bilioni moja kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA) kufanikisha utanuzi wa chujio la maji na kupunguza kero ya mgawo wa maji kwa wateja wa maji mjini Geita.
Meneja Ufundi wa Geuwasa, Mhandisi Izack Mgeni ametoa taarifa hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita baada ya kufika na kukagua mradi na kuelezea upanuzi wa chujio utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita laki mbili hadi lita laki 3.5 kwa saa.
Amesema upanuzi wa chujo hilo unafanyika katika chanzo kikuu cha maji mjini Geita kilichopo Nyankanga ambacho kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha wastani wa lita milioni nne kwa siku ikilinganishwa na mahitaji ya lita milioni 18 kwa siku.
Amesema maboresho yataongeza uzalishaji wa maji kwa siku kutoka milioni nne mpaka milioni saba na kuongeza masaa ya upatikanaji wa huduma kutoka masaa 12 kwa sasa mpaka masaa 18 kwa siku kwa wananchi waliopo kwenye mtandao.
“Mradi huu unahusisha ujenzi wa miundombinu ya kutibu maji lakini pia tuna ununuzi wa pampu kubwa ambayo itaondosha haya maji kupeleka matenki ya mjini ambapo upanuzi wa chujio una gharama ya Sh milioni 812 Kwa upande wa ununuzi wa pampu unagharimu kiasi cha Sh milioni 199. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi novemba kwa mjibu wa mpango kazi wa mkandarasi na tunazidi kumusihi kila siku akamilishe mradi kwa wakati.” Mhandisi Mgeni.
Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Wakandarasi wa Mradi ambao ni GIPCO, Keneth Sindiro amesema utekelzaji wa mradi umeanza mwezi aprili mwaka huu, wapo kwenye hatua nzuri na wanapambana kukamilisha kari ya mkataba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Geuwasa, Mhandisi Frank Changawa amesema mradi huo ni wa dharura ili kupunguza kero ya maji mjini Geita huku wakisubiri utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Viktoria.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amemuagiza mkandarasi wa mradi kutekeleza kadri ya mkataba ili kusaidia kuondoa kero ya mgawo wa maji kwa wakazi mjini Geita.