Zaidi ya shilingi bilioni 2,365,005895 zimeletwa na Serikali ya awamu ya sita katika Halmashauri ya Mji Kondoa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa Ndg.Paul Mamba Sweya wakati wa mkutano na vyombo vya habari wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutangaza mafanikio ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka mitatu kwa mikoa na halmashauri iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
“Kwa kuona umuhimu wa uwepo wa vituo vya afya Serikali ya awamu ya sita imeleta shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Serya baada ya kusikia kilio cha wakazi wa kata hiyo ambapo mwaka 2021 mzazi mmoja alifariki na mtoto wake wakati akijifungua kutokana na kujaa maji kwa Mto Bubu unaounganisha kata hiyo na Kondoa Mjini ilipo hospitali kubwa,”amesema Mkurugenzi Sweya.
Ameongeza kuwa Serikali pia imeleta shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kolo na imeongeza idadi ya vituo vya afya kutoka kituo kimoja hadi kuwa na vituo vya afya 3 ambavyo vimesaidia kupunguza msongamano katika Hospitali ya Mji.
“Pia Serikali imeleta zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika mitaa sita na kupelekea kuongezeka kwa zahanati kutoka 4 hadi kufikia zahanati 10 ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa Wananchi wa maeneo hayo ambapo wananchi walikuwa wakisafiri zaidi ya kilomita 10 kutafuta huduma za afya,”amesisitiza Mkurugenzi Sweya
Ameendelea kueleza kuwa serikali kwa kuona Hospitali ya Mji ni chakavu wameleta shilingi milioni kwa ajili ya ukaratabati wa majengo ya hospitali hiyo ambapo majengo mapya ya kisasa matatu yamejengwa ambayo ni jengo la upasuaji, mama na mtoto na jengo la mochwari
“Pia kwa upande wa vifaa tiba imeleta shilingi milioni 1,265,468,504.2 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Mji na vituo vya kutolea huduma za afya ambapo kwasasa vipimo vingi vinafanyika katika maeneo hayo na watumishi wanapata ujuzi zaidi kutokana na kutumia vifaa hivyo vya kisasa,”amesema Mkurugenzi Sweya
Akitaja manufaa ya miradi hiyo amesema kuwa ni kupunguza vifo vitokanavyo na ajali za barabarani na magonjwa ya dharura, kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi, kuongeza morali ya kazi kwa watumishi kufuatia uwepo wa nyumba za watumishi na uwepo wa vifaa tiba vya kisasa, kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma za Afya.
Kampeni ya kutangaza mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita chini ya kauli mbiu “Tumekusikia Tumekufikia” imezinduliwa katika mkoa wa Dodoma ambapo imefunguliwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kufungwa na Naibu Waziri wa OR TAMISEMI Mhe. Festo Ndugange na imehudhuriwa pia Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg. Mobhare Matinyi, Mhe. Rosemary Senyamule Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa wa Dodoma.