Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr. Kuku Farmer Ltd, Tariq Machibya (29), maarufu kama Mr.Kuku, kulipa fidia ya Bilioni 5.4 baada ya kukiri mashtaka ya kushiriki katika Upatu na kupokea miamala ya fedha kutoka kwa umma.
Mr.Kuku alikuwa akikabiliwa na kesi ya kufanya biashara haramu ya upatu na kukusanya fedha za umma Bilioni 17.
Katika hukumu hiyo, pia Mahakama imemuhukumu mshtakiwa huyo kulipa faini ya Milioni 5 ama akishindwa atatumikia kifungo cha miaka mitano gerezani.
Mbali na hilo pia mahakama imeamuru fedha Bilioni 5,456,480.41 ambazo zipo katika akaunti za mshtakiwa zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali.
Na pia Mahakama hiyo imeamuru fedha hizo kuhamishiwa katika akaunti namba 9921169817 iliyoko Benki Kuu ya Tanzania kwa jina la Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Hukumu hiyo, imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya ambaye amesema Mahakama imezingatia kwamba mshtakiwa amekiri mwenyewe makosa yake na ni mkosaji wa mara ya kwanza na wameangalia makubaliano hivyo hakuna sababu ya kumpa adhabu kali.
Hata hivyo Mr.Kuku amerudishwa korokoroni kutokana na kushindwa kulipa faini hiyo kwa leo.