Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, MMwita Waitara, amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 serikali imetenga shilingi bilioni 6.0 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 20 za viongozi na bilioni 4.0 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba 40 za viongozi Jijini Dodoma.
Kauli hiyo ameitoa Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Mariam Ditopile, lililohoji mpango wa serikali katika kujenga nyumba za makazi za viongozi waandamizi wa serikali wakiwemo Makatibu Wakuu na Mawaziri Jijini humo.
“Serikali imeanza mkakati wa kujenga nyumba za viongozi katika Jiji la Dodoma na katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imetenga kiasi cha shilingi bilioni 6.0 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 20 za viongozi na shilingi bilioni 4.0 kwa ajili ya ukarabati wa nyumba 40 za viongozi Jijini Dodoma,” Naibu Waziri Waitara.