NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kufanikiwa kudhibiti matukio ya vifo na majeruhi katika shughuli za uchimbaji mgodini na kuwasisitiza waajiri wengine kuhakikisha wakati wote wanalinda usalama wa waajiriwa wao.
Biteko ametoa kauli hiyo jana Jumapili baada ya kutembelea banda la GGML katika maonesho ya afya na usalama mahali pa kazi yanayoendelea kwenye viwanja vya General Tyre jijini Arusha.
Biteko ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonesho hayo, ameeleza kufurahishwa na elimu ya afya na usalama mahali pa kazi inayotolewa na washiriki wa maonesho hayo.
“Niwapongeze wale mliofanya maonesho hapa, mmetoa elimu kubwa kwangu na kwale ambao tumepita lakini tumejifunza bado zipo kazi za kufanya,” alisema.
Alisema waajiriwa wanatakiwa kuzingatia usalama na afya mahali pa kazi kwani kifo cha mtu mmoja kwa takwimu ni sawa na asilimia 100 kwa wategemezi wake ambao ni mke, watoto, ndugu na hata majirani.
“Kifo cha mtu mmoja ni kikubwa kinatakiwa kisitokee. Wito kwa waajiri wote wakati wote nataka mhakikishe mnarekod ziro katika matukio haya ya vifo mahali pa kazi.
“Kwa waajiriwa wito wangu kwenu ni kwamba mtu wa kwanza kulinda usalama ni muajiriwa mwenyewe, ukiona mtambo unaopaswa kuundesha na una kasoro huku ukiwa umelazimishwa na muajiri kuuendesha, uwe wa kwanza kusema mtambo huu haupo salama na usihesabike kuwa mtu uliyegoma kwa sababu pia una wajibu kulinda usalama wako,” alisema.
Alidha alitoa wito kwa kila mtu kuthamini maisha yake kwamba pindi anapokuja kazini anarejea salama bila kuwa na madhara yoyote.
Awali akimkaribisha Dk. Biteko katika banda la GGML, Meneja Usalama wa kampuni hiyo Isack Senya kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 hapajawahi kutokea tukio la vifo kwa mfanyakazi akiwa kazini.
“Tuna miaka zaidi ya sita hakuna mtu aliyeumia akashindwa kurudi kazini siku inayofuata. Suala la msingi tunajitahidi kujifunza kwa wenzetu na kuendelea kuboresha maingira ya afya na usalama mahali pa kazi,” alisema.
Aidha, Senya pia alimueleza Dk. Biteko namna GGML inavyotumia mfumo wa rada kuangalia mienendo ya miamba au kuta katika maeneo ya uchimbaji.
Pia alimueleza kuwepo kwa chumba maalumu cha uokozi ambacho huwepo chini ya ardhi katika migodi ili kufanya uokozi pindi kunapotokea dharura yoyote.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama mahali pa kazi (OSHA), Hadija Mwenda alisisitiza kuwa wataendelea kusimamia majukumu yao ipasavyo kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa.
“Tutaendelea kuhamasisha kuwezesha maeneo ya kazi yawe salama. Suala la usalama na afya ni suala la kujenga tabia na ujengaji tabia ni jambo linatokana na kuelimishwa,” alisema.