Wataalamu katika Idara ya ENT ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto mdogo kwa siku sita.
Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo wa BMH, Emmerenceana Mahulu, amesema BMH imempokea mtoto huyo wa miaka miwili siku ya Alhamisi ya tarehe 26, Machi.
“Tumefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto kwa siku sita kwa kutumia kifaa tiba kinachoitwa _esophagoscopy_,” amesema Daktari huyo Bingwa ambaye pia Kaimu Mkuu wa Idara ya ENT ya BMH.
Dkt Mahulu amefafanua kuwa sehemu ya koo ilipokuwa imekwama sarafu ilisabisha uvimbe, akiongeza kuwa ilikuwa imeacha uwazi kidogo ambayo ilikuwa ikiruhusu vimiminika kama uji, maji juisi kupita.
“Mtoto anaendelea vizuri baada ya matibabu na anaweza kula vizuri kwa sasa. Tumeishamruhusu na tutamuona tena baada ya wiki moja ili kuona maendeleo yake,” amesema.
Kwa mujibu wa mama wa mtoto, Juliana Yuda, mkazi wa kijiji cha Mkoka, Kongwa, Dodoma, mtoto wake, ambaye alitoka kucheza na wenzake siku ya Jumamosi ya tarehe 20, Machi, alirudi nyumbani muda wa mchana akiwa analia.