Baadhi ya Madereva pikipiki maarufu Bodaboda Wilayani Geita wamesusia kuuzika mwili wa Bodaboda mwenzao, Abeli Dotto Mkazi wa Mtaa wa Nyantorotoro aliyefariki Dunia baada ya kuugua muda mfupi wakisema chanzo cha kususia mwili ni baadhi ya Viongozi wao kushindwa kutoa fedha za rambirambi katika baadhi ya misiba ambayo imetokea hivi karibuni ukiwemo msiba wa Abeli huku wakiwashutumu Viongozi wao kula fedha hizo.
Baadhi ya Madereva hao wameiambia @AyoTV_ kuwa Uongozi wao umeshindwa kutoa fedha za rambirambi za kumzika Abeli wakati Viongozi hao wamekuwa wakichangisha fedha Madereva za kukuza Chama na kusaidiana lakini linapotokea suala la misiba hawajishughulishi wala kutoa rambirambi jambo ambalo limewapa hasira na kuamua kuandamana wakiwa na mwili wa Abeli na kuuacha mwili huo katika ofisi za Chama chao hadi Viongozi wachangie rambirambi.
Manjale Magambo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Geita ambapo amefika katika eneo hilo na kukuta vurugu hizo na kuamua kuingilia kati ili kutuliza ghasia hizo kwa kutoa shilingi laki 5.
Baada ya kupewa laki 5 Bodaboda wamekubali kwenda kuzika mwenzao lakini wamefunga Ofisi za Chama hicho na kuwataka Viongozi wao wasiingie hadi kesho Jumapili watakapokaa kikao cha pamoja kati ya Viongozi na Madereva.