Siku moja baada ya mitandao ya millardayo kuripoti tukio la kuanguka kwa jengo la ghorofa mbili katika eneo la Magogoni Jijini Dar es Salaam na kupelekea kifo cha Fundi Omary, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amezielekeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) na Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kufika mara moja eneo la tukio na kushirikiana na timu za Wataalamu kutoka Mamlaka nyingine za Serikali kupata sababu ya kuanguka jengo hilo na kuchukua hatua stahiki kwa wote ambao wamekiuka Sheria za kitaaluma katika ujenzi na usimamizi wa jengo hilo.
Bashungwa amezitaka Bodi hizo kuhakikisha wanaendelea kusimamia miradi ya ujenzi ikiwemo barabara, madaraja na majengo na kuhakikisha Wajenzi na Wasimamizi wa miradi hiyo wanafanya kazi kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma zao.
Waziri Bashungwa ametoa pole kwa majeruhi ambao ni Mafundi wanane waliokuwa wanajenga jengo hilo na ametoa pooe pia kwa Familia iliyopoteza Mpendwa wao na ametoa wito kwa Wakandarasi, Wahandisi na wamiliki wa majengo kuhakikisha wanatumia Wataalamu waliosajiliwa na Bodi za CRB, ERB na AQRB ili kuepusha kutokea kwa madhara yanayoweza kusababisha majeruhi na vifo, na hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Itakumbukwa Afisa Zimamoto Wilaya ya Kigamboni , Mkaguzi Innocent Kirway Ingbertus akiwa eneo la tukio Wilayani Kigamboni jana April 17,2024 aliiambia @AyoTV_ kwamba ghorofa liliporomoka wakati Mafundi wengine wakiwa juu na wengine chini hivyo kupelekea kufunikwa na mmoja ambaye alikuwa eneo hatarishi lenye shimo alifunikwa na zege na kufariki “Mkandarasi wa ujenzi aliondoka eneo la tukio na hajarudi hadi sasa, Mmiliki wa jengo pia hajafika eneo la tukio”