Wizara ya Maliasili na utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imekabidhi vifaa mbalimbali vya michezo kwa Timu za Taifa za Vijana za mpira wa kikapu zitakazoshiriki mashindano ya kimataifa nchini Uganda. Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika ofisi za TTB jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Felix John amesema ufadhili huo una lengo la kutangaza utalii wa Tanzania kupitia Michuano ya Kufuzu Mashindano ya Mpira wa Kikapu kwa Nchi za Afrika kwa vijana chini ya miaka 18, ambayo yanahusisha nchi mbalimbali za Bara la Afrika.
“TTB inaendeleza programu maalum ya Royal Tour ambayo imeasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ufadhili wa jezi zilizoandikwa “Visit Tanzania”, ili kuwashawishi na kuwavutia watalii kutoka nchi za Afrika kuvitembelea vivutio vya utalii vya Tanzania’
Felix amefafanua kuwa, TTB imetoa vifaa vyenye thamani ya shilingi 6,766,120.00 ambavyo ni jozi 48 za jezi za mpira wa kikapu, Jozi 35 za “track suit” na jozi 48 za soksi ili kufanikisha ushiriki wa timu hizo na kuweza kupeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano hayo.
Kwa upande wake Rais wa Mpira wa Kikapu Tanzania, Michel Kadebe ameishukuru Wizara hiyo kwa kutoa mchango wa vifaa hivyo ambayo vimetolewa katika muda muafaka na kuhakikishia umma kwamba vijana hao wanaweza kushikiri mashindano hayo na kurudi na ushidi.
‘Tunatarajia kuondoka na wachezaji 12 wa kike na wa kiume 12 ambao tumejiridhisha wamepata maandalizi mazuri, hivyo katika mashindano haya tunatarajia kurudi na ushindi, alisema Kadebe.
Mashindano hayo ya kimataifa yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 13 hadi Juni 18 mwaka 2022 Jijini Kampala Uganda.