Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) leo May 22, 2018 wamezungumza na waandishi wa habari na kutoa malalamiko yao dhidi ya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/19 uliotolewa na Bodi ya Mikopo mwanzoni mwa mwezi huu wa tano.
Mkurugenzi wa haki za kutetea wanafunzi Gibson Johsonn Eliaform ameipongeza Bodi ya mikopo kwa kuboresha baadhi ya mambo lakini pia ametoa malalamiko kwa kusema Bodi hiyo imeendelea kubadilisha vigezo kila mwaka na kuweka vigezo visivyo na tija ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa kukwepa majukumu ya kusaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao za kupata elimu.
Gibson ameyaeleza baadhi ya malalamiko kuwa ni kipengele no.(vii) kilichotolewa na Bodi ya Mikopo kinachozuia mwanafunzi ambaye mzazi au mlezi wake kama ni mmiliki wa biashara au Meneja wa makampuni yanayotambuliwa na mamlaka kwamba hawataruhusiwa kuomba mkopo, vile vile kipengele kingine ni kile kinachomzuia wanafunzi waliotajwa katika sheria ya utumishi wa umma wasiombe mikopo.