Waziri wa Nishati January Makamba amesema kwa miaka mingi Tanzania tumekua na bomba linalojulikana kama TAZAMA lililojengwa miaka ya 1960 ambalo lilikua likisafirisha mafuta ghafi na kwenda kusafishwa kwenye kituo cha kusafisha mafuta ghafi Nchini Zambia ambapo baada ya kusimama kwa kuingiza mafuta ghafi imekubalika kubadilisha mfumo badala ya kusafirisha mafuta ghafi yasafirishwe mafuta yaliyosafishwa na mchakato huo umekamilika mwezi wa kwanza mwaka huu kwa sasa bomba hilo linasafirisha mafuta ya Dizeli na sio mafuta ghafi kama ilivyokua hapo awali.
Baada ya kuanza kusafirisha Dizeli kwenye bomba la mafuta hali ya usalama na mahitaji ya usalama ya bomba hilo yameongezeka sababu ni rahisi watu kushawishika kutoboa bomba hilo na kuchukua Dizeli, Waziri Makamba amesema ‘Tumeshafanya mkutano wa kwanza mwaka jana tuliweka makubaliano ya kuweza kulilinda bomba hili lenye urefu wa KM 1,710 kutoka Kigamboni – Dar es salaam hadi Indeni – Ndola Zambia’ – Waziri Makamba.
Kwa upande mwingine Waziri Makamba amesema>> ‘Kikao tunachokutana kitapokea taarifa ya utekelezaji wa bomba hilo na mapendekezo ya ujenzi wa bomba jipya katika mkuza huo, bomba hili limejengwa muda mrefu na lina kipenyo chembaba biashara ya mafuta imekua na mahitaji ya mafuta yamekua zaidi, kuna haja ya kujenga bomba pana na jipya litakalosafirisha pia bidhaa nyingine zaidi ya Dizeli, Serikali zote mbili zimekua zikiongea kuhusu biashara hii ya mafuta na ujenzi wa bomba jipya la gesi ili kuiuzia Zambia Gesi’ – Waziri Makamba.
Haya ni mashirikiano mazuri kati ya nchi zetu hizi na pia ni mwendelezo wa mahusiano mema unaofanywa na Viongozi wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia kama yalivyoasisiwa na Viongozi wetu wa kwanza Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na Hayati Kenneth Kaunda.