Baada ya utafiti wa muda mrefu na majadiliano yaliyochukua zaidi ya mwaka mmoja shirikisho la soka ulimwenguni limefikia uamuzi wa kutofanyika kwa mashindano ya kombe la dunia kwa mwaka 2022 katika kipindi cha msimu wa kiangazi .
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa FIFA Jerome Valcke huenda michezo ya kombe la dunia isifanyike kwa msimu huo nchini Qatar kutokana na hali ya hewa kuwa joto kali na hivyo kuhatarisha afya na usalama wa wachezaji.
Kwa muda mrefu FIFA imekuwa ikifanya utafiti kufuatia malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya mataifa kuhusiana na ugumu wa michezo ya kombe la dunia kufanyika nchini Qatar wakati wa msimu wa kiangazi ambapo hali ya hewa ni nyuzi joto 38 mpaka 40 mazingira ambayo hayawezi kutumika kwa mechi za soka hasa kwa timu za ulaya .
FIFA imetangaza kuwa huenda mashindano ya kombe la dunia kwa mwaka 2022 yakafanyika kati ya Novemba tarehe 15 na January 15 katika wakati ambao msimu utakuwa wa baridi.
Maamuzi haya yakipita huenda yakazua utata miongoni mwa wadau na wadhamini wa Mashindano haya ikiwemo kampuni ya Fox Sports ya Marekani ambayo imeingia mkataba na FIFA wa kurusha matangazo ya michezo ya kombe la dunia katika msimu wa joto huku wakiwa na mikataba ya kurusha matangazo ya michezo mingine katika msimu wa baridi.