Leo March 2018 Video Queen, Agnes Gerald maarufu ‘Masogange’ ameshindwa kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza HUKUMU ya kesi yake ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam kwa sababu amelazwa hospitalini amewekewa Dripu na hawezi kutembea.
Hayo yameelezwa na Mdhamini wa Masogange, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa serikali, Adolf Mkini kueleza kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya hukumu.
Mdhamini wa Masogange, alisimama na kumueleza Hakimu Mashauri kuwa Masogange ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu anaumwa.
“Masogange anaumwa yupo hospital amelezwa na kuwekewa Drip, pia hawezi hata kutembea,” -mdhamini.
Katika kesi hiyo, Masogange anawakilishwa na Wakili Ruben Simwanzi ambaye ameeleza kuwa mteja wake anaumwa.
Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Mashauri ameahirisha hukumu hadi April 3,2018.
Awali katika ushahidi wake Masogange alidai kuwa hajawahi kutumia dawa za kulevya, hivyo anaiomba Mahakama imuachie huru kwa sababu hana kosa.
Masogange anadaiwa kuwa kati ya February 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).
Pia anadaiwa kuwa kati ya February 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.