Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 anaripotiwa kuwagharimu Seagulls pauni milioni 16 ($20 milioni) na amesaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza.
Verbruggen alitawazwa mchezaji bora wa msimu katika klabu ya Anderlecht msimu uliopita licha ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza mwezi Desemba pekee.
Aliwasaidia wababe hao wa Ubelgiji kutinga robo fainali ya Ligi ya Mikutano ya Europa na akaitwa kwenye kikosi cha wakubwa cha Uholanzi kwa mara ya kwanza mwezi Machi.
Brighton walimaliza katika nafasi ya sita kwenye Premier League msimu uliopita na kufuzu kwa soka la Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Lakini meneja Roberto De Zerbi alimtoa mchezaji wa kimataifa wa Uhispania Robert Sanchez kama nambari moja wake katikati mwa msimu kwa ajili ya uwezo wa Jason Steele wa kupiga pasi kutoka nyuma.
“Nimefurahishwa sana kumsajili Bart,” De Zerbi alisema. “Amezoea kucheza aina ya soka linalofanana na letu na hatakuwa na tatizo kuingia kwenye kundi letu.
“Ana uwezo wa kuwa mchezaji muhimu sana kwa klabu katika miaka ijayo.”
Verbruggen anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na Brighton katika dirisha hili la usajili, kufuatia fowadi wa Brazil Joao Pedro na viungo James Milner na Mahmoud Dahoud.