Bunge la Denmark limepitisha mswada wa sheria inayoharamisha vitendo vya kuvunjia heshima nakala za Qur’ani Tukufu katika maeneo ya umma.
Vitendo kadhaa vya kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu nchini Denmark miezi ya hivi karibuni vilizua hasira miongoni mwa Waislamu katika majira ya kiangazi.
Muswada huo uliopitishwa Alhamisi unakataza “vitendo visivyofaa kwa maandishi yenye umuhimu mkubwa wa kidini kwa jumuiya ya kidini inayotambulika.”
Muswada huo ulilipitishwa kwa kura 94 za ndio na 77 za la katika bunge hilo lenye viti 179.
Kuchoma, kurarua, au kunajisi maandishi ya kidini hadharani kunaweza kusababisha watu kutozwa faini au kufungwa hadi miaka miwili gerezani. Kuharibu maandishi matakatifu kwenye video na kusambaza video mtandaoni pia kunaweza kupelekea mhusika au wahusika kufungwa jela.
Waziri wa Sheria Peter Hummelgaard amezungumza baada ya kupitishwa muswada huo na kusema: “Lazima tulinde usalama wa Denmark na Wadenmark,”
Kabla ya sheria kuanza kutekelezwa, Malkia Margrethe anahitaji kutia sahihi mswada huo.
Mswada huo, uliotangazwa mwishoni mwa Agosti, ulifanyiwa marekebisho baada ya kukosolewa kwamba rasimu yake ya kwanza inabana uhuru wa kujieleza na itakuwa vigumu kutekelezwa.