Ombi hilo la kupigwa marufuku kwa TikTok nchini Kenya limewasilishwa bungeni likitaja uvunjaji wa kanuni ya faragha na maudhui ya ngono, tovuti ya kibinafsi ya Star iliripoti.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema ombi hilo lililowasilishwa na Bob Ndolo, lilidai kuwa TikTok ilikuwa ikikusanya data muhimu kutoka kwa watumiaji wake, ikiwa ni pamoja na eneo na historia ya kuvinjari.
Mlalamishi pia amesema jukwaa hilo “linakuza vurugu, lugha chafu, maudhui ya ngono na matamshi ya chuki”.
Aliongeza kuwa programu hiyo ya mitandao ya kijamii yenye makao yake nchini China ilikuwa ikishiriki taarifa za watumiaji na makampuni ya wahusika wengine bila idhini.
Hata hivyo, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alipinga marufuku ya TikTok na akiomba mlalamishi kuzingatia udhibiti wa programu hiyo.
Serikali mnamo tarehe 2 Agosti ilisema kwamba itapitia sheria za mtandao ili kudhibiti utiririshaji wa moja kwa moja ya TikTok wakati wa usiku ambapo watumiaji wanadaiwa kupeperusha maudhui ya lugha chafu.
Kenya inaongoza ulimwenguni kwa matumizi ya TikTok.