Waziri wa ulinzi nchini Burikina Faso ametangaza kuwasimamisha kazi maafisa kadhaa wa jeshi, ambapo hakuna sababu za kusimishwa kwao zilizowekwa wazi ndani ya barua iliosainiwa na Kanali Meja Kassoum Coulibaly.
Uamuzi wa kusimishwa kazi kwa maafisa hao ulichukuliwa tangu jumatano iliopita siku ambayo mkuu wa jeshi na Polisi alipoondolewa na kuteuliwa afisa mwingine kwenye nafasi hiyo, lakini taarifa imewekwa wazi saa 24 baadae.
Waliosimamishwa kazi ni maafisa wanane akiwemo kanali mmoja, maluteni Kanali watatu na makamanda wanne, pamoja na maafisa watatu na maafisa wawili wasaidizi na sajenti mmoja.
Licha ya waziri wa Ulinzi kutotoa sababu za kusimamishwa huko, chanzo kilicho karibu jeshi kinaonyesha kuwa uamuzi huu unahusishwa na jaribio la hivi karibuni la kuyumbisha usalama.
“Watu hawa wanashukiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi lililotibuka,” kinaeleza chanzo hicho.
Maafisa wengine wa jeshi wamekimbia wakiwemo wanachama wawili wa zamani wa idara ya ujasusi pamoja na Luteni Kanali Roméo Djassanou Ouoba.