Utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso jana Jumatano ulitoa pasi mpya za kusafiri za kibayometriki bila ya kuwemo nembo yoyote ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).
Maafisa wa serikali ya Burkina Faso wametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, pasipoti hizo zina chip ya kielektroniki kwa ajili ya kukusanya na kuhifadhi data.
Mahamadou Sana, Waziri wa Usalama wa Burkina Faso amesema: “Utambulisho huu mpya utaruhusu usajili mtandaoni na kutuma data papo hapo kwa balozi za nchi hiyo kama ambavyo pia usalama wake umeongezeka.”
Aidha amesema: Pasipoti za zamani ni halali na zitaendelea kutumika hadi muda wake utakapoisha. Wale wanaotafuta pasi mpya za kusafiria watalipa ada kulingana na kiwango kilichowekwa hapo awali cha faranga 50,000 za CFA za Afrika Magharibi ($84.46). Kampuni ya Uchina ya Emptech ndiyo iliyopewa tenda ya kutengeneza pasipoti hizo mpya.
Taarifa hiyo pia imesema: “Paspoti mpya ni ya kizazi cha karibuni kabisa cha pasi zilizopendekezwa na mamlaka ya kimataifa ya usafiri wa anga. Mchakato huo ulianzishwa mwaka 2022 na unaifanya Burkina Faso kuwa nchi ya kwanza Afrika Magharibi na ya 10 barani Afrika kupata hati ya utambulisho wa hali ya juu kama hiyo.”
Mwaka jana Burkina Faso, Mali na Niger zilijiondoa katika jumuiya ya ECOWAS, ambayo ilitishia kuingilia kijeshi katika nchi hizo baada ya kutokea mapinduzi huko Niger mwezi Julai 2023.