Nchini Burundi, baada ya siku nne za mjadala kuhusu uhalali wa kesi hiyo, upande wa mashtaka siku ya Alhamisi uliomba kifungo cha maisha jela dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Alain-Guillaume Bunyoni, na kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya washtakiwa wenzake sita.
Wote wanashitakiwa kwa pamoja na mambo mengine kuhatarisha usalama wa ndani wa Serikali. Inadaiwa walipanga njama dhidi ya Rais Evariste Ndayshimiye.
Kulingana na mwendesha mashtaka wa umma, Waziri Mkuu wa zamani Alain-Guillaume Bunyoni aliajiri “watu ili kumuua mkuu wa nchi” na “kupindua utawala wa kikatiba” kwa kutumia uchawi. Lakini maelezo machache yalitolewa katika kesi iliyofungwa siku ya Jumanne.
Miongoni mwa washitakiwa wenzake, anayefahamika zaidi ni Désiré Uwamahoro, kamanda wa zamani wa kikosi cha kuzuia fujo. Afisa mkuu wa zamani wa huduma ya kijasusi, madereva wawili, mhandisi wa zamani wa majengo na mkuu wa kata pia wanashtakiwa.
Alain-Guillaume Bunyoni, mwenye umri wa miaka 51, ambaye mara nyingi alichukuliwa kuwa nambari 2 katika serikali iliyotokana na uasi wa zamani wa CNDD-FDD, alihifadhi nyumbani kwake pesa nyingi, kulingana na upande wa mashitaka, kwa lengo la “kuyumbisha kiwango cha ubadilishaji fedha (Faranga ya Burundi)” cha serikali.